11. Kisha utamchinja huyo ng’ombe mbele ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania.
12. Kisha twaa baadhi ya damu ya ng’ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu.
13. Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu.
14. Lakini nyama yake huyo ng’ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya marago; ni sadaka kwa ajili ya dhambi.
15. Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume.
16. Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando.
17. Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake.
18. Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya BWANA; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
19. Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo.
20. Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando.