1. Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwatakasa, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa ng’ombe mmoja mume kijana, na kondoo waume wawili walio wakamilifu,
2. na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano.
3. Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng’ombe, na hao kondoo waume wawili.
4. Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji.
5. Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi;
6. nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba.
7. Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta.
8. Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu.
9. Nawe uwakaze mishipi, Haruni na wanawe, na kuwavika kofia; nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele; nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu.
10. Kisha utamleta huyo ng’ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng’ombe.
11. Kisha utamchinja huyo ng’ombe mbele ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania.
12. Kisha twaa baadhi ya damu ya ng’ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu.
13. Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu.