Kut. 23:12-19 Swahili Union Version (SUV)

12. Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng’ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.

13. Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.

14. Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu.

15. Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu;

16. tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani.

17. Mara tatu katika mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU.

18. Usisongeze damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hata asubuhi.

19. Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya BWANA, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

Kut. 23