1. Mtu akiiba ng’ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng’ombe watano badala ya ng’ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.
2. Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake.
3. Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake.
4. Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng’ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili.
5. Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake.
6. Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa.
7. Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwivi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili.
8. Mwivi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe.