22. Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa.
23. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi.
24. Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu.
25. Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani.
26. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.
27. Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione.
28. BWANA akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini?
29. Angalieni, kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.
30. Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba.
31. Na nyumba ya Israeli wakakiita jina lake Mana; nacho kilikuwa mfano wa chembe za mtama, nyeupe; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya maandazi membamba yaliyoandaliwa kwa asali.
32. Musa akasema, Hili ni neno BWANA aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri.
33. Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya BWANA, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu.
34. Kama vile BWANA alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe.