Kut. 15:4-18 Swahili Union Version (SUV)

4. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini,Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.

5. Vilindi vimewafunikiza,Walizama vilindini kama jiwe.

6. BWANA, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo,BWANA, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui.

7. Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea,Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu.

8. Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa,Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu,Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

9. Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara,Nafsi yangu itashibishwa na wao;Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza.

10. Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza;Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu.

11. Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe?Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu,Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?

12. Ulinyosha mkono wako wa kuume,Nchi ikawameza.

13. Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa,Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.

14. Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka,Wakaao Ufilisti utungu umewashika.

15. Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa,Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata,Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka.

16. Hofu na woga umewaangukia;Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe;Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA,Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

17. Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako,Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae,Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako.

18. BWANA atatawala milele na milele.

Kut. 15