Kut. 12:18-31 Swahili Union Version (SUV)

18. Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni.

19. Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi.

20. Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.

21. Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka.

22. Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi.

23. Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi.

24. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele.

25. Itakuwa hapo mtakapoifikilia hiyo nchi, BWANA atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu.

26. Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N’nini maana yake utumishi huu kwenu?

27. Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia.

28. Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama BWANA alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.

29. Hata ikawa, usiku wa manane BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama.

30. Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu.

31. Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni BWANA kama mlivyosema.

Kut. 12