1. Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni,
2. watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki?
3. Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA.
4. Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako.
5. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
6. Basi jua ya kuwa BWANA, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.
7. Kumbuka, usisahau ulivyomtia BWANA, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya BWANA
8. Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza.
9. Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji.
10. BWANA akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi BWANA mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano.
11. Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, BWANA alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano.
12. BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.