5. Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.
6. Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako; BWANA Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.
7. BWANA hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote;
8. bali kwa sababu BWANA anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu BWANA akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.
9. Basi jueni ya kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu;
10. naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake.
11. Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazokuamuru leo, uzitende.
12. Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi BWANA, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako;
13. naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng’ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.
14. Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo.
15. Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.
16. Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa BWANA, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.
17. Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?
18. Usiwaogope; kumbuka sana BWANA, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;
19. uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.
20. Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.