Kum. 7:12-26 Swahili Union Version (SUV)

12. Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi BWANA, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako;

13. naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng’ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa.

14. Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo.

15. Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.

16. Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa BWANA, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.

17. Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?

18. Usiwaogope; kumbuka sana BWANA, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;

19. uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.

20. Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.

21. Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho.

22. Naye BWANA, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu.

23. Ila BWANA, Mungu wako, atawatoa mbele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa.

24. Na wafalme wao atakutilia mkononi mwako, nawe utalipoteza jina lao litoke chini ya mbingu; hapana mtu atakayeweza kusimama mbele yako, hata utakapokwisha kuwaangamiza.

25. Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako;

26. na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.

Kum. 7