Kum. 6:6-19 Swahili Union Version (SUV)

6. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;

7. nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

8. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.

9. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.

10. Tena itakuwa atakapokwisha BWANA, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe,

11. na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba;

12. ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.

13. Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.

14. Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;

15. kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.

16. Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa.

17. Zishikeni kwa bidii sheria za BWANA, Mungu wenu, na mashuhudizo yake, na amri zake alizokuagiza.

18. Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa BWANA; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri BWANA aliyowaapia baba zako,

19. ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema BWANA.

Kum. 6