Kum. 31:6-17 Swahili Union Version (SUV)

6. Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana BWANA, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.

7. Musa akamwita Yoshua, akamwambia machoni pa Israeli wote, Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana utakwenda pamoja na watu hawa hata nchi BWANA aliyowaapia baba zao, ya kwamba atawapa; nawe utawarithisha.

8. Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.

9. Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, wana wa Lawi, waliolichukua sanduku la agano la BWANA, na wazee wote wa Israeli.

10. Musa, akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda,

11. Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za BWANA, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya Israeli wote masikioni mwao.

12. Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha BWANA, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii;

13. na watoto wao wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha BWANA, Mungu wenu, siku zote mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki.

14. BWANA akamwambia Musa, Tazama, siku zako za kufa zinakaribia, umwite Yoshua, nanyi mkajihudhurishe katika hema ya kukutania, ili nipate kumwagiza kazi. Musa na Yoshua wakaenda, wakajihudhurisha ndani ya hema ya kukutania.

15. BWANA akaonekana katika Hema katika nguzo ya wingu; na ile nguzo ya wingu ikasimama juu ya mlango wa Hema.

16. BWANA akamwambia Musa, Angalia, wewe utalala na baba zako; na watu hawa wataondoka, wataifuata kwa ukahaba miungu ya kigeni ya nchi waiendeayo kuwa kati yao, nao wataniacha mimi na kulivunja agano langu, nililofanya nao.

17. Ndipo hasira yangu itakapowaka juu yao siku hiyo, nami nitawaacha, nitawaficha uso wangu, nao wataliwa, tena watajiliwa na mambo maovu mengi na mashaka; hata waseme siku hiyo, Je! Kujiliwa kwetu na maovu haya si kwa sababu Mungu wetu hayumo kati yetu?

Kum. 31