1. Ndipo tukageuka, tukakwea njia ya Bashani; na Ogu, mfalme wa Bashani, akatutokea juu yetu, yeye na watu wake wote, kuja kupigana huko Edrei.
2. BWANA akaniambia, Usimwogope; kwa kuwa nimemtia mkononi mwako, yeye na watu wake wote na nchi yake; nawe utamtenda mfano wa ulivyomtenda Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni.
3. Basi BWANA, Mungu wetu, akamtia mikononi mwetu na Ogu mfalme wa Bashani, na watu wake wote; tukampiga, asisaziwe cho chote.
4. Tukatwaa miji yake yote wakati huo; hapakuwa na mji tusiotwaa kwao miji sitini, nchi yote ya Argobu, ndio ufalme wa Ogu ulio katika Bashani.
5. Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma marefu, na malango, na makomeo, pamoja na miji isiyokuwa na maboma, mingi sana.
6. Tukaiharibu kabisa, kama tulivyomfanya huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, kwa kuharibu kabisa kila mji uliokuwa na watu, pamoja na wanawake na watoto.
7. Lakini wanyama wote wa mji, na nyara za miji, tulitwaa kuwa mawindo yetu.
8. Tukaitwaa na nchi wakati huo, katika mikono ya hao wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ng’ambo ya Yordani, tokea bonde la Arnoni mpaka kilima cha Hermoni;
9. (na hiyo Hermoni Wasidoni huiita Sirioni, na Waamori huiita Seniri);
10. miji yote ya nchi tambarare, na Gileadi yote, na Bashani yote, mpaka Saleka na Edrei, nayo ni miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani.
11. (Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho je! Hakiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni mikono kenda, na upana wake mikono minne, kwa mfano wa mkono wa mtu).