15. Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.
16. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.
17. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.
18. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
19. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,
20. BWANA atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.
21. BWANA atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.
22. BWANA atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.
23. Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.
24. BWANA atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.