Kum. 28:12-29 Swahili Union Version (SUV)

12. Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.

13. BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;

14. msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.

15. Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.

16. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.

17. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.

18. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

19. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,

20. BWANA atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.

21. BWANA atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.

22. BWANA atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.

23. Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.

24. BWANA atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.

25. BWANA atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani.

26. Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza.

27. BWANA atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa.

28. BWANA atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni;

29. utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.

Kum. 28