Kum. 24:8-22 Swahili Union Version (SUV)

8. Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao.

9. Kumbukeni na BWANA, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri.

10. Umkopeshapo jirani yako cho chote kikopeshwacho usiingie katika nyumba yake kwenda kutwaa rehani kwake.

11. Simama nje, yule umkopeshaye akuletee nje ile rehani.

12. Naye akiwa ni mtu maskini, usilale na rehani yake.

13. Sharti umrudishie rehani lichwapo jua, apate kulala na mavazi yake, na kukubarikia; nayo itakuwa ni haki kwako mbele za BWANA, Mungu wako.

14. Usimwonee mtumishi mwenye ujira aliye maskini na uhitaji, kama ni wa nduguzo, au kama ni wageni wako mmojawapo walio katika nchi yako, ndani ya malango yako;

15. mpe ujira wake kwa siku yake, wala jua lisichwe juu yake; kwa maana ni maskini, moyo wake umeutumainia huo; asije akamlilia BWANA juu yako, ikawa ni dhambi kwako.

16. Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.

17. Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani;

18. bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, BWANA, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.

19. Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili BWANA, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako.

20. Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.

21. Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane.

22. Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.

Kum. 24