4. yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za BWANA; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi.
5. Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa.
6. Mtu awaye yote asitwae jiwe la kusagia, la juu wala la chini, kuwa rehani; kwani hivi ni kutwaa maisha ya mtu kuwa rehani.
7. Mtu akionekana anamwiba nduguze mmojawapo katika wana wa Israeli, akamfanya kama mtumwa, au kumwuza; na afe mwivi huyo; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
8. Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao.
9. Kumbukeni na BWANA, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri.
10. Umkopeshapo jirani yako cho chote kikopeshwacho usiingie katika nyumba yake kwenda kutwaa rehani kwake.
11. Simama nje, yule umkopeshaye akuletee nje ile rehani.
12. Naye akiwa ni mtu maskini, usilale na rehani yake.
13. Sharti umrudishie rehani lichwapo jua, apate kulala na mavazi yake, na kukubarikia; nayo itakuwa ni haki kwako mbele za BWANA, Mungu wako.