1. Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake, kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake.
2. Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine.
3. Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha, na kumpa mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa, aliyemtwaa kuwa mkewe;
4. yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za BWANA; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi.
5. Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa.
6. Mtu awaye yote asitwae jiwe la kusagia, la juu wala la chini, kuwa rehani; kwani hivi ni kutwaa maisha ya mtu kuwa rehani.
7. Mtu akionekana anamwiba nduguze mmojawapo katika wana wa Israeli, akamfanya kama mtumwa, au kumwuza; na afe mwivi huyo; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
8. Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao.
9. Kumbukeni na BWANA, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri.
10. Umkopeshapo jirani yako cho chote kikopeshwacho usiingie katika nyumba yake kwenda kutwaa rehani kwake.