1. Umwonapo ng’ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea, usijifiche kama usiyemwona; sharti utamrudisha kwa nduguyo.
2. Na kwamba yule nduguyo hayupo karibu nawe, au ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie.
3. Tena fanya vivyo kwa punda wake; tena fanya vivyo kwa mavazi yake; tena fanya vivyo kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo, kilichompotea ukakiona wewe; usijifiche kama usiyekiona.
4. Umwonapo punda wa nduguyo, au ng’ombe wake, ameanguka kando ya njia, usijifiche kama usiyemwona; sharti umsaidie kumwinua tena.
5. Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako.
6. Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;
7. sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi.
8. Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko.
9. Usipande shamba lako la mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako.
10. Usilime kwa ng’ombe na punda wakikokota jembe pamoja.
11. Usivae nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja.
12. Ujifanyizie vishada katika pembe nne za mavazi yako ya kujifunika.
13. Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia,
14. kisha akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira;
15. ndipo babaye yule kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee wa mji langoni;
16. na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa binti yangu awe mkewe, naye amchukia;
17. angalieni, amemwekea mambo ya aibu, asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji.
18. Basi wazee wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi,