3. Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako.
4. Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote; wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni, kisilale cho chote usiku kucha hata asubuhi.
5. Usimchinje pasaka ndani ya malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako;
6. ila mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.
7. Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako.
8. Siku sita utakula mikate isiyotiwa chachu; na siku ya saba na uwe mkutano mtukufu kwa BWANA, Mungu wako, usifanye kazi yo yote.
9. Jihesabie majuma saba; tangu wakati uanzao kutia mundu katika mmea utaanza kuhesabu majuma saba.
10. Nawe sikukuu ya majuma umfanyie BWANA, Mungu wako, kwa kutoa sadaka ya hiari ya mkono wako, utakayotoa kwa kadiri akubarikiavyo BWANA, Mungu wako;
11. nawe utafurahi mbele ya BWANA, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake.