16. Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako;
17. ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi chako naye mfanye vivyo.
18. Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na BWANA, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya.
19. Wazaliwa wa kwanza waume wote wazaliwao katika kundi lako la ng’ombe na la kondoo, uwatakase kwa BWANA, Mungu wako; usifanye kazi kwa mzaliwa wa kwanza wa ng’ombe wako, wala usimkate manyoya mzaliwa wa kwanza wa kundi lako la kondoo.
20. Utamla mbele za BWANA, Mungu wako, mwaka hata mwaka mahali atakapochagua BWANA, wewe na nyumba yako.
21. Lakini akiwa na kilema, akichechea, au akiwa kipofu, au mwenye kilema kibaya cho chote, usimsongezee BWANA, Mungu wako, sadaka.
22. Utamla ndani ya malango yako; wasio tohara na wenye tohara pia watakula, kama unavyokula paa na kulungu.
23. Pamoja na haya usile damu yake; uimwage nchi kama maji.