Kum. 12:1-13 Swahili Union Version (SUV)

1. Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa BWANA, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi.

2. Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;

3. nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.

4. Wala msimfanyie hivyo BWANA, Mungu wenu.

5. Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko;

6. pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo;

7. na huko mtakula mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia BWANA, Mungu wako.

8. Msifanye kwa kufuata mambo yote tuyafanyayo hapa leo, kila mtu kama aonavyo vema machoni pake;

9. kwani hamjafikilia bado katika raha na urithi akupao BWANA, Mungu wako.

10. Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha BWANA, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama;

11. wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa BWANA.

12. Nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu.

13. Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;

Kum. 12