Kum. 10:3-16 Swahili Union Version (SUV)

3. Basi nikafanya sanduku la mti wa mshita, nikachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, nikakwea mle mlimani, na zile mbao mbili mkononi mwangu.

4. Naye akaandika juu ya mbao mfano wa maandiko ya kwanza, zile amri kumi, alizowaambia BWANA huko mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano; BWANA akanipa.

5. Basi nikageuka nikashuka kutoka mlimani, nikazitia mbao ndani ya sanduku nililofanya; nazo zimo humo kama alivyoniamuru BWANA.

6. (Wana wa Israeli wakasafiri kutoka visima vya Bene-Yaakani kwenda Mosera; Haruni akafa huko, akazikwa huko; na Eleazari mwanawe alitumika utumishi wa ukuhani badala yake.

7. Wakasafiri kutoka huko kwenda Gudgoda; wakatoka Gudgoda wakaenda Yotbatha, nayo ni nchi ya vijito vya maji.

8. Na wakati huo BWANA aliitenga kabila ya Lawi ili walichukue lile sanduku la agano la BWANA, wasimame mbele ya BWANA kwa kumtumikia, na kuwabarikia watu kwa jina lake, hata hivi leo.

9. Ndipo asiwe na fungu Lawi, wala urithi pamoja na nduguze; BWANA ndiye urithi wake, kwa mfano wa vile alivyomwambia BWANA, Mungu wako.)

10. Nikakaa mle mlimani kama hapo kwanza, siku arobaini usiku na mchana; BWANA akanisikiza wakati huo nao; asitake BWANA kukuangamiza.

11. BWANA akaniambia, Ondoka, ushike safari yako mbele ya watu; nao wataingia waimiliki nchi, niliyowaapia baba zao ya kuwa nitawapa.

12. Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;

13. kuzishika amri za BWANA na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri?

14. Tazama, mbingu ni mali za BWANA, Mungu wako, na mbingu za mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo.

15. Tena, BWANA aliwafurahia baba zako, na kuwapenda, akawachagua wazao wao baada yao, naam, na ninyi zaidi ya mataifa yote kama hivi leo.

16. Basi, zitahirini govi za mioyo yenu, wala msiwe na shingo ngumu.

Kum. 10