Kum. 1:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. ni ng’ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema,

6. BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha;

7. geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati.

8. Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao.

9. Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu.

10. BWANA, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi.

11. BWANA, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi.

12. Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na mateto yenu?

13. Jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya kabila zenu, nami nitawafanya wawe vichwa juu yenu.

14. Nanyi mkanijibu, mkaniambia, Jambo ulilonena ni jema la kufanya.

15. Basi nikatwaa vichwa vya kabila zenu wenye akili, waliojulikana, nikawafanya wawe vichwa juu yenu, maakida ya elfu elfu, na maakida ya mia mia, na maakida ya hamsini hamsini, na maakida ya kumi kumi, na wenye amri, kwa kadiri ya kabila zenu.

16. Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye.

17. Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza.

18. Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya.

Kum. 1