Kum. 1:17-36 Swahili Union Version (SUV)

17. Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza.

18. Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya.

19. Tukasafiri kutoka Horebu, tukapita katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha mliloliona, njia ile ya kuiendea nchi ya vilima vya Waamori, kama BWANA, Mungu wetu, alivyotuamuru, tukafika Kadesh-barnea.

20. Nami nikawaambia, Mmefika nchi ya vilima ya Waamori, anayotupa sisi BWANA, Mungu wetu.

21. Tazama, BWANA, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike.

22. Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.

23. Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila.

24. Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza.

25. Wakatwaa baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa BWANA, Mungu wetu, ni nchi njema.

26. Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la BWANA, Mungu wenu;

27. mkanung’unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza.

28. Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki.

29. Ndipo nikawaambieni, Msifanye hofu, wala msiwache.

30. BWANA, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu;

31. na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua BWANA, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafikilia mahali hapa.

32. Lakini katika jambo hili hamkumwamini BWANA, Mungu wenu,

33. aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonyesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu.

34. BWANA akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema,

35. Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa,

36. isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata BWANA kwa kila neno.

Kum. 1