Kum. 1:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Haya ndiyo maneno Musa aliyowaambia Israeli wote ng’ambo ya Yordani barani, katika Araba lililoelekea Sufu, kati ya Parani, na Tofeli, na Labani, na Hazerothi, na Dizahabu.

2. Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya mlima wa Seiri mpaka Kadesh-barnea.

3. Ikawa mwaka wa arobaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na BWANA ya kuwaamuru;

4. alipokwisha kumpiga Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa akikaa Ashtarothi iliyo katika Edrei;

5. ni ng’ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema,

6. BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha;

7. geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati.

8. Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao.

9. Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu.

Kum. 1