Isa. 66:10-19 Swahili Union Version (SUV)

10. Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake;

11. mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake.

12. Maana BWANA asema hivi, Tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa.

13. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu.

14. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa BWANA utajulikana, uwaelekeao watumishi wake, naye atawaonea adui zake ghadhabu.

15. Maana BWANA atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto.

16. Kwa maana BWANA atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na BWANA watakuwa wengi.

17. Watu wale wajitakasao, na kujisafisha katika bustani, nyuma yake aliye katikati; wakila nyama ya nguruwe, na machukizo, na panya; watakoma pamoja, asema BWANA.

18. Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu.

19. Nami nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, Tarshishi, na Puli, na Ludi, wavutao upinde, kwa Tubali na Yavani, visiwa vilivyo mbali; watu wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika mataifa.

Isa. 66