11. Bali ninyi mmwachao BWANA, na kuusahau mlima wangu mtakatifu, na kuandika meza kwa ajili ya Bahati, na kuijazia Ajali vyombo vya divai iliyochanganyika;
12. mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga, na ninyi nyote mtainama ili kuchinjwa; kwa sababu nilipoita hamkuitika; niliponena, hamkusikia; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia.
13. Kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, watumishi wangu watakula, bali ninyi mtaona njaa; tazama, watumishi wangu watakunywa, bali ninyi mtaona kiu; tazama, watumishi wangu watafurahi, bali ninyi mtatahayarika;
14. tazama, watumishi wangu wataimba kwa furaha ya moyo, bali ninyi mtalia kwa huzuni ya moyo; mtapiga kelele kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.
15. Nanyi mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa wateule wangu. Na Bwana MUNGU atakuua; naye atawaita watumishi wake kwa jina lingine.
16. Hata itakuwa yeye atakayejibariki duniani, atajibariki kwa Mungu wa kweli; naye atakayeapa duniani, ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za kwanza zimesahauliwa, na kwa kuwa zimefichwa machoni pangu.
17. Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.
18. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.
19. Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.
20. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.
21. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.
22. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.
23. Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao.