Isa. 65:1-11 Swahili Union Version (SUV)

1. Watu wasionitaka wanauliza habari zangu; nimeonekana na hao wasionitafuta; naliliambia taifa lisiloitwa kwa jina langu,

2. Nitazameni, nitazameni. Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao katika njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe;

3. watu wanikasirishao mbele za uso wangu daima, wakitoa dhabihu katika bustani zao, na kufukiza uvumba juu ya matofali;

4. waketio kati ya makaburi, na kulala katika mahali pao pa siri; walao nyama ya nguruwe, na mchuzi wa vitu vinichukizavyo u katika vyombo vyao;

5. watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.

6. Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu. Sitanyamaza, lakini nitalipa, naam, mimi nitawalipa ujira wao vifuani mwao;

7. maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema BWANA, ninyi mliofukiza uvumba juu ya milima, na kunitukana juu ya vilima; basi, kwa ajili ya hayo nitawapimia kwanza kazi yao vifuani mwao.

8. BWANA asema hivi, Kama vile divai mpya ipatikanavyo katika kichala, na mtu mmoja husema, Usikiharibu kwa maana mna baraka ndani yake; ndivyo nitakavyotenda kwa ajili ya watumishi wangu, ili nisiwaharibu wote.

9. Nami nitaleta uzao toka Yakobo, na mrithi wa milima yangu toka Yuda, na mteule wangu atairithi, na watumishi wangu watakaa huko.

10. Na Sharoni itakuwa zizi la makundi ya kondoo, na bonde la Akori mahali pa kulala makundi ya ng’ombe, kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.

11. Bali ninyi mmwachao BWANA, na kuusahau mlima wangu mtakatifu, na kuandika meza kwa ajili ya Bahati, na kuijazia Ajali vyombo vya divai iliyochanganyika;

Isa. 65