7. Nitautaja wema wa BWANA, sifa za BWANA kwa yote aliyotukirimia BWANA; na wingi wa wema wake kwa nyumba ya Israeli, aliowakirimia kwa rehema zake, na kwa wingi wa wema wake.
8. Maana alisema, Hakika ndio watu wangu hawa, wana wasio na hila; akawa Mwokozi wao.
9. Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.
10. Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.
11. Ndipo alipozikumbuka siku za kale, za Musa, na watu wake, akisema, Yuko wapi yeye aliyewapandisha toka baharini pamoja na wachungaji wa kundi lake? Yuko wapi yeye aliyetia kati yao Roho yake Mtakatifu?
12. Aliyewaongoza kwa mkono wake mtukufu, kwa mkono wa kuume wa Musa? Aliyeyatenga maji mbele yao, ili ajifanyie jina la milele?
13. Aliyewaongoza vilindini, kama farasi jangwani, wasijikwae?
14. Kama ng’ombe washukao bondeni, Roho ya BWANA akawastarehesha; ndivyo ulivyowaongoza watu wako, ili ujifanyie jina lenye utukufu.