Isa. 57:11-21 Swahili Union Version (SUV)

11. Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi?

12. Mimi nitatangaza haki yako, na matendo yako hayatakufaa.

13. Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali; lakini yeye anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu.

14. Naye atasema,Tutieni, tutieni,Itengenezeni njia,Kiondoeni kila kikwazachoKatika njia ya watu wangu.

15. Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.

16. Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya.

17. Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake naliona hasira, nikampiga; nalificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe.

18. Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.

19. Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema BWANA; nami nitamponya.

20. Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka.

21. Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.

Isa. 57