Isa. 57:1-7 Swahili Union Version (SUV)

1. Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya.

2. Yeye huingia katika amani; wao hustarehe katika vitanda vyao, kila mtu aendaye katika unyofu wake.

3. Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi, uzao wa mzinzi na kahaba.

4. Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani? Mmepanua vinywa vyenu, na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo;

5. ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi; ninyi mnaoua watoto mabondeni, chini ya mianya ya majabali?

6. Sehemu yako i katika makokoto ya bonde; hayo ndiyo kura yako; umeyamwagia hayo sadaka ya kinywaji, umeyatolea sadaka ya unga; je! Niwe radhi na mambo hayo?

7. Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu.

Isa. 57