Isa. 54:10-17 Swahili Union Version (SUV)

10. Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema BWANA akurehemuye.

11. Ewe uliyeteswa, uliyerushwa na tufani, usiyetulizwa, tazama, nitaweka mawe yako kwa rangi nzuri, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.

12. Nami nitaifanya minara yako ya akiki nyekundu, na malango yako ya almasi, na mipaka yako yote ya mawe yapendezayo.

13. Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.

14. Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.

15. Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.

16. Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu.

17. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.

Isa. 54