Isa. 51:15-23 Swahili Union Version (SUV)

15. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma.

16. BWANA wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.

17. Amka, amka, simama, Ee Yerusalemu,Wewe uliyenywea, mkononi mwa BWANA,Kikombe cha hasira yake;Bakuli la kikombe cha kulevya-levyaUmelinywea na kulimaliza.

18. Hapana hata mmoja wa kumwongozaMiongoni mwa wana wote aliowazaa,Wala hapana hata mmoja wa kumshika mkonoMiongoni mwa wana wote aliowalea.

19. Mambo haya mawili yamekupata;Ni nani awezaye kukusikitikia?Ukiwa na uharibifu, na njaa na upanga;Niwezeje kukutuliza?

20. Wana wako wamezimia,Wamelala penye pembe za njia kuu zoteKama kulungu wavuni;Wamejaa hasira ya BWANA,Lawama ya Mungu wako.

21. Basi, kwa sababu ya hayo, ulisikilize neno hili, ewe uliyeteswa, na kulewa, lakini si kwa mvinyo;

22. BWANA, Bwana wako na Mungu wako, awateteaye watu wake, asema hivi, Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe cha kulevya-levya, hilo bakuli la kikombe cha hasira yangu; hutakinywea tena;

23. nami nitakitia mikononi mwao wakutesao; waliokuambia nafsi yako, Inama, tupate kupita; nawe uliufanya mgongo wako kuwa kama nchi, na kama njia, kwa hao wapitao juu yake.

Isa. 51