Isa. 51:11-22 Swahili Union Version (SUV)

11. Nao waliokombolewa na BWANA watarejea,Watafika Sayuni, wakiimba;Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao;Watapata shangwe na furaha;Huzuni na kuugua zitakimbia.

12. Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani?

13. Ukamsahau BWANA, Muumba wako, yeye aliyezitanda mbingu, na kuiweka misingi ya dunia; nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo afanyapo tayari kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye?

14. Yeye aliyehamishwa na kufungwa atafunguliwa kwa haraka; wala hatakufa na kushuka shimoni, wala chakula chake hakitapunguka.

15. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma.

16. BWANA wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.

17. Amka, amka, simama, Ee Yerusalemu,Wewe uliyenywea, mkononi mwa BWANA,Kikombe cha hasira yake;Bakuli la kikombe cha kulevya-levyaUmelinywea na kulimaliza.

18. Hapana hata mmoja wa kumwongozaMiongoni mwa wana wote aliowazaa,Wala hapana hata mmoja wa kumshika mkonoMiongoni mwa wana wote aliowalea.

19. Mambo haya mawili yamekupata;Ni nani awezaye kukusikitikia?Ukiwa na uharibifu, na njaa na upanga;Niwezeje kukutuliza?

20. Wana wako wamezimia,Wamelala penye pembe za njia kuu zoteKama kulungu wavuni;Wamejaa hasira ya BWANA,Lawama ya Mungu wako.

21. Basi, kwa sababu ya hayo, ulisikilize neno hili, ewe uliyeteswa, na kulewa, lakini si kwa mvinyo;

22. BWANA, Bwana wako na Mungu wako, awateteaye watu wake, asema hivi, Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe cha kulevya-levya, hilo bakuli la kikombe cha hasira yangu; hutakinywea tena;

Isa. 51