1. BWANA asema hivi, Iko wapi hati ya talaka ya mama yenu, ambayo kwa hiyo naliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani katika watu wanaoniwia? Ninyi mliuzwa kwa sababu ya maovu yenu; tena mama yenu ameachwa kwa sababu ya makosa yenu.
2. Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je! Mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je! Mimi sina nguvu za kuponya? Tazama, kwa kukemea kwangu naikausha bahari, mito ya maji naifanya kuwa jangwa; samaki wao wanuka kwa sababu hapana maji, nao wafa kwa kiu.
3. Mimi nazivika mbingu weusi, nami nafanya nguo ya magunia kuwa kifuniko chao.
4. Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao.
5. Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma.
6. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate.
7. Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.
8. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi.