9. BWANA wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu.
10. Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu.
11. Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao!
12. Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya BWANA wala kuyafikiri matendo ya mikono yake.
13. Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana.
14. Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.
15. Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa,
16. bali BWANA wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki.