14. Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo.
15. Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa,
16. bali BWANA wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki.
17. Ndipo wana-kondoo watakapolisha kama katika malisho yao wenyewe, na mahali pao waliowanda, palipoachwa ukiwa, wageni watakula.
18. Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari!
19. Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona.
20. Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu!
21. Ole wao walio wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe!
22. Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, watu waume wenye nguvu kuchanganya vileo;
23. wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake!
24. Kwa hiyo kama vile mwali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika mwali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli.