13. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi;Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima;Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake,Naye atawahurumia watu wake walioteswa.
14. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.
15. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.
16. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.
17. Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako.
18. Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema BWANA, hakika utajivika na hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi.
19. Maana katika habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali.
20. Watoto ulionyang’anywa watasema masikioni mwako, Mahali hapa ni pembamba, hapanitoshi; nipe nafasi nipate kukaa.
21. Ndipo utasema moyoni mwako, Ni nani aliyenizalia watoto hawa, na mimi nimefiwa na watoto wangu, nami ni peke yangu, nimehamishwa, ninatanga-tanga huko na huku? Tena ni nani aliyewalea hawa? Tazama, naliachwa peke yangu; hawa je! Walikuwa wapi?
22. Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainulia mataifa mkono wangu, na kuwatwekea kabila za watu bendera yangu; nao wataleta wana wako vifuani mwao, na binti zako watachukuliwa mabegani mwao.
23. Na wafalme watakuwa baba zako za kulea, na malkia zao mama zako za kulea; watainama mbele yako kifudifudi, na kuramba mavumbi ya miguu yako; nawe utajua ya kuwa mimi ni BWANA, tena waningojeao hawatatahayarika.
24. Je! Aliye hodari aweza kunyang’anywa mateka yake, au jeshi lao waliofungwa halali wataokoka?
25. Naam, BWANA asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu.
26. Na hao wanaokuonea nitawalisha nyama yao wenyewe, nao watalewa kwa kuinywa damu yao wenyewe, kama kwa mvinyo mpya; na wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako, na Mkombozi wako ni Mwenye enzi wa Yakobo.