Isa. 49:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; BWANA ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu.

2. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha;

3. akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.

4. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina BWANA, na thawabu yangu ina Mungu wangu.

5. Na sasa BWANA asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya BWANA, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu);

6. naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

7. BWANA, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya BWANA aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua

8. BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa;

9. kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho.

10. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.

11. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote.

12. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu.

13. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi;Pazeni sauti ya kuimba, enyi milima;Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake,Naye atawahurumia watu wake walioteswa.

14. Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.

15. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.

16. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.

Isa. 49