Isa. 44:23-28 Swahili Union Version (SUV)

23. Imbeni, enyi mbingu, maana BWANA ametenda hayo;Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi;Pazeni nyimbo, enyi milima;Nawe, msitu, na kila mti ndani yake.Maana BWANA amemkomboa Yakobo,Naye atajitukuza katika Israeli.

24. BWANA, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?

25. Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;

26. nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;

27. niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;

28. nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.

Isa. 44