Isa. 44:18-28 Swahili Union Version (SUV)

18. Hawajui wala hawafikiri; maana amewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu.

19. Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti?

20. Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu?

21. Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi.

22. Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa.

23. Imbeni, enyi mbingu, maana BWANA ametenda hayo;Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi;Pazeni nyimbo, enyi milima;Nawe, msitu, na kila mti ndani yake.Maana BWANA amemkomboa Yakobo,Naye atajitukuza katika Israeli.

24. BWANA, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?

25. Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;

26. nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;

27. niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;

28. nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.

Isa. 44