7. Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.
8. Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu;
9. wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa;
10. usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
11. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia.
12. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.
13. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.
14. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli.
15. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi.
16. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.
17. Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, BWANA, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.
18. Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.