1. Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.
2. Mfalme wa Ashuru akamtuma amiri toka Lakishi hata Yerusalemu, kwa mfalme Hezekia, pamoja na jeshi kubwa. Naye akasimama karibu na mfereji wa birika ya juu, iliyo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.
3. Wakamtokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.
4. Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kwamba mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?
5. Nasema, mashauri yako, na nguvu zako kwa vita, ni maneno yasiyo na maana; basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?
6. Tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo, mtu akitegemea juu yake, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.
7. Lakini ukiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu, je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii?
8. Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.
9. Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi?
10. Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza.
11. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani.
12. Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?