Isa. 33:1-6 Swahili Union Version (SUV)

1. Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.

2. Ee BWANA, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asububi, na wokovu wetu pia wakati wa taabu.

3. Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.

4. Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.

5. BWANA ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.

6. Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha BWANA ni hazina yake ya akiba.

Isa. 33