1. Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu.
2. Na mwanadamu atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba; kama mito ya maji mahali pakavu, kama kivuli cha mwamba mkubwa katika nchi yenye uchovu.
3. Tena macho yao waonao hayatakuwa na kiwi, na masikio yao wasikiao yatasikiliza.
4. Tena moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu maarifa, na ndimi zao wenye kigugumizi zitakuwa tayari kunena sawasawa.
5. Mpumbavu hataitwa tena mwungwana, wala ayari hatasemwa kwamba ni karimu.
6. Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya BWANA, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa hazina kitu, na kukikomesha kinywaji chake mwenye kiu.
7. Tena vyombo vyake ayari ni vibaya; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki.
8. Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana.
9. Inukeni, enyi wanawake wenye raha, isikieni sauti yangu; enyi binti za watu msiokuwa na uangalifu, tegeni masikio yenu msikie matamko yangu.
10. Maana mtataabishwa siku kadha wa kadha zaidi ya mwaka, enyi wanawake mliojikinai; kwa sababu mavuno ya mizabibu yatakoma, wakati wa kuvuna vitu vya mashamba hautakuja.
11. Tetemekeni, enyi wanawake wenye raha; taabikeni, enyi msiokuwa na uangalifu; jivueni, jivueni nguo zenu kabisa, jivikeni viuno nguo za magunia.
12. Watajipiga vifua kwa ajili ya mashamba mazuri, kwa ajili ya mzabibu uliozaa sana.