Isa. 30:22-33 Swahili Union Version (SUV)

22. Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa.

23. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana.

24. Ng’ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.

25. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara.

26. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile BWANA atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.

27. Tazama, jina la BWANA linakuja kutoka mbali sana, linawaka kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana unaopaa juu; midomo yake imejaa ghadhabu, na ulimi wake ni moto ulao;

28. na pumzi yake ni kijito kifurikacho, kifikacho hata shingoni, kupepeta mataifa kwa ungo wa ubatili; na lijamu ikoseshayo itakuwa katika taya za watu.

29. Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo na filimbi katika mlima wa BWANA, aliye Mwamba wa Israeli.

30. Naye BWANA atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonyesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto ulao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu.

31. Maana kwa sauti ya BWANA, Mwashuri atavunjika-vunjika, yeye apigaye kwa bakora.

32. Na kila pigo la fimbo iliyoamriwa, ambayo BWANA ataliweka juu yake, litakuwa pamoja na matari na vinanda, na kwa mapigano yenye kutikisa atapigana nao.

33. Maana Tofethi imewekwa tayari tokea zamani, naam, imewekwa tayari kwa mfalme huyo; ameifanya kubwa, inakwenda chini sana; tanuru yake ni moto na kuni nyingi; pumzi ya BWANA, kama mto wa kiberiti, huiwasha.

Isa. 30