Isa. 24:11-23 Swahili Union Version (SUV)

11. Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka.

12. Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu.

13. Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake.

14. Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini.

15. Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.

16. Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana.

17. Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani.

18. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika.

19. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana.

20. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena.

21. Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia;

22. nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa.

23. Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.

Isa. 24