Isa. 19:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Ufunuo juu ya Misri. Tazama, BWANA amepanda juu ya wingu jepesi, anafika Misri; na sanamu za Misri zinatikisika mbele zake, na moyo wa Misri unayeyuka ndani yake.

2. Nami nitawaamsha Wamisri juu ya Wamisri; nao watapigana, kila mtu na ndugu yake, na kila mtu na jirani yake, mji juu ya mji, na ufalme juu ya ufalme.

3. Na roho ya Misri itamwagika kabisa katikati yake, nami nitayabatilisha mashauri yake, nao watakwenda kwa sanamu zao, na kwa waganga, na kwa wapiga ramli, na kwa wachawi.

4. Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, BWANA wa majeshi.

5. Na maji ya baharini yatapunguka, na huo mto utakauka na kuwa pakavu.

6. Na vijito vya mto vitatoa uvundo, na mifereji ya Misri itakuwa haina maji mengi, itakauka; manyasi na mianzi itanyauka.

7. Vitu vimeavyo karibu na Nile, katika ukingo wa Nile, na vyote vilivyopandwa karibu na Nile vitakauka na kuondolewa na kutoweka.

8. Na wavuvi wataugua, na wote wavuao kwa ndoana watahuzunika, nao watandao jarife juu ya maji watazimia.

9. Tena wao wafanyao kazi ya kuchana kitani watafadhaika, na hao pia wafumao bafta.

10. Na nguzo za nchi zitavunjika vipande vipande, wote wafanyao kazi ya mshahara watahuzunika nafsini mwao.

11. Wakuu wa Soani wamekuwa wapumbavu kabisa; washauri wenye hekima wa Farao, shauri lao limepumbazika; mwawezaje kumwambia Farao, Mimi ni mwana wa wenye hekima, ni mwana wa wafalme wa zamani?

12. Wako wapi, basi, watu wako wenye hekima? Na wakuambie sasa; na wajue mambo aliyokusudia BWANA wa majeshi juu ya Misri.

Isa. 19