7. Katika siku hiyo mwanadamu atamwangalia Muumba wake, na macho yake yatamtazama Mtakatifu wa Israeli.
8. Wala hataziangalia madhabahu, kazi ya mikono yake; wala hatavitazama vilivyofanyika kwa vidole vyake, maashera na sanamu za jua.
9. Katika siku hiyo miji yake yenye maboma itakuwa kama mahali palipoachwa ndani ya mwitu, na juu ya kilele cha mlima, palipoachwa mbele ya wana wa Israeli; napo patakuwa ganjo.
10. Maana umemsahau Mungu wa wokovu wako, wala hukuukumbuka mwamba wa ngome yako; kwa sababu hiyo ulipanda mashamba yapendezayo, na kutia ndani yake mizabibu migeni.